Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hayati Ayatollah Mohammad Ali Naseri, mmoja wa Maprofesa wa Maadili wa Hawza, alijadili mada ya: "Kiasi, ni njia ya furaha katika mafundisho ya Kiislamu" katika moja ya masomo yake ya Maadili (Akhlaq), ambayo maandiko yake ni kama ifuatavyo:
Imam Sajjad (amani iwe juu yake) anasema katika Dua yenye thamani ya al-Akhlaq Nzuri (Maadili Mema):
«اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَی مُحَمَّدٍ وَآلِهِ وَمَتِّعْنِی بِالاقْتِصَادِ».
Katika kifungu hiki, Imam anamwomba Mwenyezi Mungu ambariki Muhammad na Familia yake kwa mafanikio ya (Kiasi) Wastani katika mambo yote.
Katika utamaduni wa Kiislamu, neno "uchumi" lina maana zaidi ya maana yake ya kawaida katika lugha ya Kiajemi. Ingawa katika Kiajemi cha kisasa, neno hili limejitolea zaidi kwa masuala ya mali na fedha, katika Lugha ya Kiarabu na Utamaduni wa Kiislamu, maana yake ni (Wastani) Kiasi katika nyanja zote za Maisha; limechukuliwa kutoka kutembea njiani na kuzungumza, mpaka kuwa ibada na riziki.
Katika Surat Luqman, Qur’an Tukufu inazungumza kupitia ulimi wa mtu huyu mwenye Hekima ya Kimungu ambaye anamhutubia mwanawe akisema:
«وَاقْصِدْ فِي مَشْیِكَ وَاغْضُضْ مِنْ صَوْتِكَ».
Aya hii yenye heshima inaeleza wazi kwamba hata wakati wa kutembea njiani, mtu anapaswa kuzingatia na kuheshimu mpaka wa kati (Kiasi) – kwa maana atembee kwa mwendo wa wastani –; Hatakiwi kutembea kwa majivuno (mikogo, na maringo), wala kutembea polepole kwa uzembe (na uvivu).
Pia, Kiasi kinapaswa kuzingatiwa katika kuzungumza; mtu hapaswi kuzungumza kwa kupaza sauti yake juu sana, wala kuongea kwa upole (kwa sauti ya chini) sana.
Amirul Muminin Ali (amani iwe juu yake) katika wosia wake wa busara kwa Mwanawe Imam Hassan (amani iwe juu yake) anasema:
«وَ اقْتَصِدْ یَا بُنَيَّ فِي مَعِیشَتِكَ وَاقْتَصِدْ فِي عِبَادَتِك».
Katika wosia huu, anaonyesha “Kiasi” katika maeneo mawili muhimu ya Maisha: Riziki na Ibada. Katika masuala ya Fedha (Pesa au Mali), hupaswi kufanya israfu (kutumia hovyo na kupoteza) wala kuwa bahili. Matajiri wanapaswa kujua kwamba Mwenyezi Mungu amewapa mali (pesa) hii, ili waweze kuwajali na kuwatunza wahitaji (masikini na mafakiri).
Katika suala hili, Hadhrat Ali (amani iwe juu yake) anasema:
«إِنَّ اَللَّهَ فَرَضَ فِي أَمْوَالِ اَلْأَغْنِیَاءِ أَقْوَاتَ اَلْفُقَرَاءِ».
Imam Ali (a.s) anasisitiza katika maneno haya kwamba Matajiri ni Mawakala (au Mawakili) wa Mwenyezi Mungu na Maskini ni Familia yake, na ikiwa Matajiri watashindwa katika jukumu hili, adhabu ya kimungu itawangojea.
“Kiasi” kinapaswa pia kuzingatiwa katika uwanja wa Ibada. Kuabudu kupita “Kiasi” katika ibada ya Mustahabu, kunaweza kusababisha ubaridi na uchovu wa ibada.
Inashauriwa kugawanya siku katika sehemu kuu tatu:
Sehemu ya kutafuta riziki.
Sehemu ya ibada.
Na sehemu ya kupumzika.
Katika Qur'an Tukufu , Mwenyezi Mungu anaonyesha kuwa “usingizi wa usiku” ni moja ya ishara Zake:
«وَمِنْ آیَاتِهِ مَنَامُکُمْ بِاللَّیْلِ».
Kuhusu kufunika, Amirul-Mu’minin anasema pia katika Khutba yake maarufu kwa jina la “Khutba ya Wacha Mungu” (akizitaja sifa bora za Wacha Mungu):
«وَمَلْبَسُهُمُ الإقْتِصَادُ».
Nguo za watu Wacha Mungu si za anasa sana, wala si nguo rahisi sana, bali ni za kawaida na za uwiano (za kiasi na wastani).
Your Comment