Hawzah News Agency - Kulingana na parstoday, waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio alitangaza uamuzi huo jana Ijumaa katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X akisema kwamba: Rasool "hakubaliwi tena katika nchi yetu kubwa, ni mwanasiasa mbabe ambaye anaichukia Marekani na anayemchukia Rais wa Marekani (POTUS)."
Haya yanajiri baada ya Rasool kushiriki katika mkutano wa taasisi ya wanafikra wa Afrika Kusini ambapo alisema kuwa kampeni ya Trump ya 'Make America Great Again' (Kuifanya Marekani Bora Tena), pamoja na ushawishi wa Elon Musk na Makamu wa Rais J.D. Vance, ni sehemu ya mtindo wa kimataifa wa kuhudumia wasiwasi (maslahi) ya Wazungu.
Aidha alisema kuwa Trump alitumia "silika ya upendeleo" na "ubaguzi wa rangi" kama "filimbi ya mbwa" wakati wa uchaguzi wa 2024.
Tangu Trump arejee ofisini, Balozi huyo wa Afrika Kusini ameripotiwa kuzuiwa kushiriki mikutano ya kawaida ya kidiplomasia na maafisa wa Marekani.
Matamshi ya Rubio yanaashiria kuzorota zaidi kwa mahusiano ya Marekani na Afrika Kusini, ambayo tayari yaliingia doa kutokana na msimamo wa Pretoria kuhusu haki za Wapalestina.
Hivi karibuni, Naibu Katibu Mkuu wa Kwanza wa chama tawala cha Afrika Kusini, ANC, Nomvula Mokonyane, akizungumza pambizoni mwa mkutano wa chama hicho uliofanyika Free State, aliunga mkono kauli ya Rais Cyril Ramaphosa kwamba Afrika Kusini haitakubali kutishwa na Marekani.
Your Comment