Saturday 15 March 2025 - 10:56
Mpango wa Qur'ani wa Watoto Wazinduliwa Bainul Haramayn katika Mwezi wa Ramadhani

Kituo cha Qur'ani cha Idara ya Mfawidhi wa Haram ya Hadhrat Abbas (AS) kimezindua toleo la tatu la mpango wake maalum wa Qur'ani kwa watoto na vijana katika eneo la Bainul Haramayn, Karbala.

Shirika la Habari la Hawza Hafla hiyo inayofanyika kwa mnasaba wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, ilianza Jumanne jioni, Machi 11, kwa uwepo wa maafisa wa eneo na mkusanyiko mkubwa wa wafanyaziyara.

Akizungumza katika hafla hiyo, Ala’ al-Mousawi, Naibu Mwenyekiti wa Mkutano wa Sayansi ya Qur'ani, alisema: "Kwa mwaka wa tatu mfululizo,  eneo la Bainul Haramayn linakaribisha mipango ya Qur'ani iliyowekwa kwa watoto."

Al-Mousawi alieleza kuwa mpango huo unalenga katika kuongeza uelewa wa watoto na vijana kuhusu mafundisho ya Qur'ani na kuwafahamisha na Qur'ani na mila za Ahl al-Bayt (AS).

"Mpango huu utadumu kwa siku kumi, ukikusanya idadi kubwa ya washiriki vijana na wafanyaziara. Shughuli mbalimbali zimepangwa ili kuwashirikisha waliohudhuria," aliongeza.

Mohannad al-Mayali, Mkurugenzi wa Taasisi ya Qur'ani huko Najaf na msimamizi wa mpango huo, aliongeza maelezo kuhusu hafla hiyo. "Shughuli hizo ni pamoja na mashindano ya Qur'ani yenye maswali kuhusu Qur'ani, maisha ya Mtume (SAW), fiqhi ya Kiislamu, imani, na maadili. Pia kuna sehemu ya kuchora ambapo washiriki wanaweza kuunda michoro inayohusiana na Ahl al-Bayt (AS), pamoja na mihadhara ya ushauri na mkazo juu ya kuhifadhi hotuba na maneno ya Imam Ali (AS) kutoka Nahjul Balagha," alibainisha.

Mpango huo unafanyika kila usiku kuanzia saa 2:30 usiku hadi saa sita usiku.

Bainul Haramayn , yaani baina ya Haram Mbili, ni eneo kati ya Haram ya Imam Hussein (AS) na Haram ya  Hadhrat Abbas (AS), ambalo lina umbali wa mita 378. Inasemekana kuwa ni mahali kamili ambapo mapigano ya Siku ya Ashura katika Vita vya Karbala yalitokea.

Chanzo: IQNA 

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha