Sunday 16 February 2025 - 19:02
Je, Umahdi unaweza kuwa daraja la mazungumzo ya kidini?

Profesa wa hawza na chuo kikuu na mtafiti wa Umahdi alisema: Umahdi ni suala la mazungumzo ya kimataifa; haliwahusu Shia pekee au hata Waislamu tu. Karibu katika dini zote na madhehebu zote, hata kwa uwepo wa tofauti kidogo tu, wote kwa ujumla wanaitikadia kuwa utafika wakati wa kudhihiri kwa mwokozi na kipindi cha dhahabu.

Kulingana na Shirika la Habari la Hawza: Majadiliano ya Umahdi yanakuzwa kama fursa ya kimataifa. Kwa ujumla, fursa na nafasi hii vinaweza kuchunguzwa katika makundi matatu: Nafasi ya Umahdi wenyewe, nafasi ya sasa na hali ya dunia, na nafasi na hali zetu wenyewe.

Tunaweza kuzichunguza fursa na nafasi hizi katika kategoria tatu za jumla. Kundi la kwanza ni nafasi ya Umahdi wenyewe, hususan Umahdi wa Ushia wa Maimamu Kumi na Wawili.

Tuna nafasi ya thamani sana ambayo hatuitilia maanani sana, nayo ni kuitikadia (na kumwamini) Imam aliye hai wakati wowote.

Tunaamini kwamba Imam wa Zama (a.t.f.s) yu hai na anasimamia matendo yetu; Imani hii inatoa matumaini maalum na nguvu kwa jamii ya Shia na inatufanya sisi daima kungojea na kudhihiri kwa Imam na mageuzi yake.

Hii ni pamoja na ukweli kwamba dini nyingine nyingi hazina imani hiyo, na viongozi wao wa kidini walikiishi zamani.

Imani hii juu ya Imam aliye Hai ni mashuhuri sana katika Madhehebu ya Shia ya Maimamu Kumi na Wawili, na kwa bahati mbaya sisi tunaizingatia (na kuipa umuhimu) kidogo nafasi hii muhimu. Kwa mfano, Henri Corben, mtafiti na Mtaalamu wa Uislamu na Mashuhuri wa Ufaransa, anaonyesha katika kazi zake kwamba imani ya kuwapo kwa Hojja wa Mwenyezi Mungu aliye Hai wakati wowote ni sifa ya pekee ya Madhehebu ya Shia inayodumisha uhusiano kati ya Mwenyezi Mungu na Mwanadamu.

Aidha, Umahdi ni suala la mazungumzo ya kimataifa; Sio kwa madhehebu ya Shia pekee au hata Waislamu tu. Karibu katika dini zote na madhehebu zote, hata kwa uwepo wa tofauti kidogo, bado wote wanaamini na kuitikadia kuwa utafika wakati wa kudhihiri kwa mwokozi na kipindi cha dhahabu.

Tunaweza kujadili hili kwa urahisi na wafuasi wa imani na dini nyingine na kutumia mfanano katika imani zetu kuhusu Mwokozi ile kujenga hali ya kufahamiana na kuhurumiana .

Umahdi ni jambo ambalo lina nafasi tatu za kimsingi:

Kwanza: Una msingi mkubwa wa kitheolojia. Tunaweza kuthibitisha Umahdi na ulazima wa (Wilayat) Mwongozo wa Mwenyezi Mungu kiakili na kwa kutumia njia ya simulizi kwa kurejelea Aya za Qur'an Tukufu na Hadithi (na Riwaya) sahihi. Usaidizi huu mkubwa wa imani ni tumaini kubwa kwa Mashia; Kwa sababu kuamini uwepo wa faraja na msaada wa Imam wa Zama (a.t.f.s) kwa upande wetu kunatupa nguvu ya ziada.

Pili: Hali ya sasa ya dunia imetoa nafasi kubwa ya kuukubali Umahdi. Dunia inakumbwa na migogoro mingi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa; Umaskini, vita, pengo la kitabaka n.k ambapo vimewatumbukiza watu katika kutafuta Mkombozi (wa Ulimwengu). Masharti haya, yanatoa mazingira mazuri ya kuwasilisha na kukubali ujumbe wa Umahdi.

Tatu: Kuongezeka (kukua) kwa Uislamu ulimwenguni kumeunda fursa nyingine ya kupanua wazo la Umahdi kwa mujibu wa takwimu za kuaminika, hata baadhi ya magazeti ya Magharibi yanaripoti kwamba Uislamu utakuwa dini ya kwanza duniani katika miaka ijayo, na ukuaji huu utaweka msingi wa kukubalika kwa wazo la ukombozi katika eneo pana la dunia.

Zaidi ya hayo, mwelekeo unaoongezeka wa masuala ya kiapokaliptiki (zama za mwsiho) na matarajio ya kudhihiri kwa Mwokozi, katika nchi za Magharibi na Mashariki, kumejenga uwezo mwingine wa kukubali Umahdi, filamu za apocalyptic (apokaliptiki) – kwa maana Filamu zinazohusu zama za mwisho – , makala na takwimu kutoka kwa taasisi mbalimbali kama vile Kituo cha Utafiti cha Pew huko Marekani, zinaonyesha ongezeko la matarajio na matumaini ya kuonekana (na kudhihiri) kwa Mwokozi baina ya watu wa dunia.

Lakini kutazama (suala hili la Umahdi kwa ngazi ya) ulimwengu tu haitoshi. Ndani ya nchi, mapenzi na imani ya watu juu ya Umahdi, licha ya matatizo ya kisiasa na kijamii, imeendelea kuwa thabiti na inaonekana wazi katika sherehe za Nusu ya Mwezi wa Sha'ban na Marasimu (Hafla) za Kimadhehebu.

Pia, katika nchi nyingi za Kiislamu kama vile Iraq, Uturuki, Tunisia, Lebanon na Pakistan, imani katika Umahdi ni kubwa sana. Imani hii inayojumuisha (mataifa mengi) inachukuliwa kuwa nukta kubwa ya matumaini ya kupanuka na kukubalika kwa Umahdi duniani kote.

Harakati za Upinzani (Muqawamah), kinyume na maoni ya baadhi ya watu, sio tu kwamba hazikupungua, lakini ikilinganishwa na miongo miwili au mitatu iliyopita, zimekuwa na uwezo na nguvu zaidi katika nchi kama Lebanon, Iraq, Yemen na Iran, na imani ya Umahdi baina ya Mashia ni imani kubwa na ya ujasiri ambayo imehamasisha harakati na maendeleo yao.

Moshe Ya'alon, waziri wa zamani wa ulinzi wa Israel hivi karibuni alisema katika makala yake iliyochapishwa katika gazeti la Los Angeles Times kwamba moja ya mambo makuu ya nguvu ya Iran ni imani ya Mwokozi na utamaduni wa ukombozi; Na akakiri kwamba imani hii ndiyo kichochezi cha hatua kubwa ambazo Iran imepiga katika njia ya maendeleo.

Nafasi hizi tatu - msingi wa kitheolojia, hali ya kimataifa na mtiririko wa Upinzani (Muqawamah) - zinaweza kutoa nguvu kubwa na uwezo wa kutambua ubora wa Umahdi duniani. Ikiwa tutazingatia nafasi hizi na kuzitumia ipasavyo, tunaweza kuzitumia kuelekea kudhihiri kwa Hadhrat Mahdi (a.t.f.s).

Bila shaka, pamoja na nafasi hizo, lazima pia tuwe waangalifu kuhusu vitisho. Vitisho mbalimbali vinaweza kuelekezwa kwetu kutoka ndani (kama vile vikundi potovu na mawazo potofu) au kutoka nje (kama vile maadui wa Umahdi katika medani ya kimataifa).

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha