Thursday 23 January 2025 - 14:35
Mashirika ya haki yaonya; Trump atarejesha marufuku dhidi ya Waislamu

Mashirika ya kutetea haki za kiraia nchini Marekani yameonya kuwa, amri ya utendaji iliyosainiwa na Rais Donald Trump siku ya Jumatatu inaweka msingi wa kurejesha marufuku ya wasafiri kutoka nchi zenye Waislamu na Waarabu wengi kuingia Marekani.

Kamati ya Kupambana na Ubaguzi ya Wamarekani Waarabu (ADC) imesema dikrii hiyo mpya inategemea mamlaka ile ile ya kisheria iliyotumiwa kuhalalisha marufuku ya kusafiri ya Trump mwaka 2017, na inatoa "uhuru mpana zaidi wa kutumia itikadi kukataa ombi la visa na kuwatimua watu ambao tayari walikuwa wameingia nchini humo. 

Nalo Baraza la Kitaifa la Wamarekani wenye asili ya Iran (NIAC) limesema agizo la Trump kuhusu "Kuilinda Marekani dhidi ya Magaidi wa Kigeni na Vitisho vingine vya Usalama wa Kitaifa na Usalama wa Umma" litatenganisha familia za Marekani na wapendwa wao, na kupunguza idadi ya wanaojiunga na Vyuo Vikuu vya Marekani.

Katika kampeni zake za urais, Trump alisisitiza kuwa, akichaguliwa atarejesha tena marufuku ya kusafiri kwa baadhi ya nchi zenye Waislamu wengi katika siku ya kwanza ya utawala wake mpya. Alisema ataweka tena marufuku ya kusafiri kwa watu kutoka eneo la Palestina la Gaza, Libya, Somalia, Syria, Yemen na "eneo lolote linapotishia usalama wetu."

Trump mwenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, akiwa madarakani, aliweka marufuku ya kusafiri kuingia Marekani kutoka nchi saba zenye Waislamu wengi duniani. Uamuzi huo uliibua maandamano na malalamiko kutoka taasisi mbali mbali kama American Civil Liberties Union. Marufuku ya kusafiri Waislamu kwenda Marekani ilikuwa sehemu yenye utata katika muhula wake wa kwanza kama rais, na ilibatilishwa na Rais Joe Biden alipoingia madarakani.

Chanzo: parstoday

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha