Thursday 27 February 2025 - 08:32
Hukumu za Kisheria kwa Mujibu wa Madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s)

Hukumu za Kisheria zitakazomfanya Mwanadamu afaulu Kesho Siku ya Kiyama, zinagawanyika katika sehemu kuu tatu: Hukumu za Kiitikadi, Hukumu za Kimatendo, na Hukumu za Kimaadili.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hojjat al-Islam wa Muslimin, Sheikh Abdul Majid Naser, ameeleza katika Darsa maalum kuhusiana na Hukumu za Kisheria kwa mujibu wa Madhehbu ya Ahlul-Bayt (a.s) kwamba Sheria hizo ndizo ambazo zitamfanya Mwanadamu aweze kufaulu Kesho Siku ya Kiyama.

Akifafanua kuhusiana na maudhui hii amesema: Sheria hizi za Kiislamu au Hukumu hizi za Kisheria zinagawanyika katika sehemu kuu tatu:

Sehemu ya Kwanza: Ni Itikadi: Muislamu inabidi uhakikishe kwamba itikadi zako zinakuwa sahihi. Qur’an Tukufu imetuletea mfumo ambao katika hatua ya kwanza kabisa unahusu suala la kiitikadi, kwa maana: Hukumu za Kiitikadi ambazo ni Usul al-Din (Misingi ya Dini).

Katika sehemu hii ya Itikadi: Hukumu za Kiislamu zinakutaka Muislamu Itikadi yako iwe ni Itikadi sahihi. Na Uislamu unatufndisha kuwa haijuzu kwa Muislamu yeyote kumfuata (Kumqalid) mtu kuhusiana na suala la Kiitikadi, kwa maana kwamba: Lolote linalohusiana na itikadi, inabidi Muislamu ulikubali na kuliitikadia kwa kutegemea dalili na uthibitisho madhubuti ima wa: Qur’an Tukufu, au Hadithi na Sunna za Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake na Aali zake) na Riwaya mbalimbali za Maimam watoharifu (amani iwe juu yao), au uwe ni uthibitisho unaotokana na dalili za kiakili.

Kwa mantiki hiyo, katika suala la kiitikadi Muislamu hutakiwi kumfuata mtu, na kama ikitokea ukamfuata mtu basi iwe ni kwa kutaka ushauri tu wa kielimu kutoka kwake, lakini ile hukumu ya mwisho kwamba mimi ninaitikadia hivi au vile, au siitikadii hivi au vile, hilo linategemea ile dalili ambayo atakuwa amekuonyesha na wewe utatakiwa kusimama katika msingi na mwongozo wa dalili hiyo.

Ikiwa utakinaika kuwa dalili hii ni sahihi na ni madhubuti juu ya jambo hili ambalo ninatakiwa niliitikadie, basi hapo utakuwa umeenda sawa katika suala zima la kufuatilia na kuitikadia masuala ya kiitikadi.

Sehemu ya Pili: Ni Hukumu za Kimatendo: Qur’an Tukufu pia imetuletea mfumo unaohusu hukumu za kimatendo, kwa maana ya (Furu’ al-Din). Hizi ni Hukumu za Kifiqh au Kisheria zinazohusiana na matendo ya Mja. Hivyo, baada ya itikadi yako kuwa sahihi, matendo yako pia yanatakiwa yaendane na hukumu za kisheria.

Katika hukumu hizi za kisheria (za Kifiqh) kuhusiana na matendo, zipo hukumu zinazoelezea kuwa baadhi ya matendo ni wajibu kutendwa katika maisha yako. Na zingine zinaeleza kuwa yapo matendo ambayo hupaswi kuyatenda. Kama Muislamu unatakiwa uyajue matendo ambayo ni wajibu kuyatenda ili uyatende, na uyajue matendo ambayo hutakiwi kuyatenda ili ujiepushe nayo. Kwa sababu msingi wa Mwenyezi Mungu katika kukulipa Thawabu na Pepo Siku ya Kiyama au Adhabu na Moto wa Jahannam, ni matendo hayo. Ikiwa yale unayotakiwa kuyatenda umeyajua na ukayatenda, maana yake yake Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atakulipa malipo mazuri na utakuwa umefaulu pamoja na wenye kufaulu. Lakini ikiwa umetenda duniani matendo ambayo hukutakiwa uyatende, Kesho Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atakuadhibu. Kwa hiyo, matendo ni msingi wa malipo yako akhera.

Hebu fikiria nukta hii kwamba: Unakwenda Akhera, sio itikadi yako ni sahihi, sio matendo ya wajibu umeyatenda, na labda zaidi utakuwa umetenda yale ambayo yamekatazwa!, Basi wewe unatakiwa ujue kuwa Akhera hutakuwa na mafanikio yoyote, bali maisha yako huko Akhera yatakuwa ni maisha ya tabu na adhabu za milele. Ili ufaulu Duniani na Akhera, Maisha yako yanatakiwa yawe katika mfumo huo wa kuyajua na kuyatambua matendo sahihi na ya wajibu kuyatenda, kisha uyatende, na uyatambue na kuyajua matendo ambayo haupaswi kamwe kuyatenda, kisha uyaepuke.

Mfano wa Matendo ya Wajibu Kuyatenda:

  1. Muislamu anatakiwa aswali: Katika Sheria ya Kiislamu, Swala ina hukumu ya Wajibu. Muslamu unapofikia umri wa kutekeleza Sheria za Kiislamu, wewe unakuwa ni Mukalaf, na Sheria inakwambia ni wajibu kwako kuswali. Ukilitambua hilo kuwa Uislamu unanitaka nitekeleza wajibu huu wa kusimamisha ibada ya Swala, na mfumo wa maisha yako ukawa ni mfumo usioacha kutelekeza wajibu huu wa Kisheria, basi wewe ujue kwamba utakuwa umepiga hatua muhimu katika maisha yako.
  2. Kutoa Zaka: Kwa maana kwamba wewe uliyetimiza wajibu wa kutoa Zaka, unapofikia wakati wa kutoa zaka, ukatoa lile fungu la kisheria na kuwapatia wanaostahiki au kulipeleka sehemu inayostahili, utakuwa umetekeleza moja wapo ya matendo ya wajibu. Hii ni baadhi tu ya mifano michache ya matendo ya wajibu.

Mfano wa Matendo Yasiyofaa Kuyatenda:

  1. Kusengenya: Katika Uislamu, tendo la kusengenya lina Hukumu ya Kisheria, nayo ni kwamba tendo hilo ni Haram kwako Muislamu kumsengenya (kumsema vibaya) mtu mwingine. Muislamu unatakiwa ujue hilo kuwa katika Uislamu ni Haram kwangu mimi kumsengenya mtu mwingine, na ujiepushe na hilo.
  2. Kuiba: Tendo la kuiba, ni kuchukua kitu cha mtu bila rukhsa yake. Katika Uislamu tendo hilo ni Haram. Kwahiyo, wewe kama Muislamu baada ya kujua hilo kuwa kuiba ni Haram, utatakiwa ujiepushe na kitendo kama hicho kibaya katika maisha yako. Ikitokea ukatenda tendo kama hilo la kuiba au kusengenya au mengine ya Haram, basi ujue kuwa Mwenyezi Mungu atakuadhibu kesho Siku ya Kiyama kwa tendo hilo ulilolifanya ambalo ni tendo la Haram.

Sehemu ya Tatu: Ni suala la Akhlaq (Maadili): Qur’an Tukufu (Uislamu) imetuletea mfumo mzuri unaohusiana na suala la maadili kwamba Muislamu maadili yako inabidi yawe vipi. Sifa za nafsi, sifa zako wewe kama wewe, unatakiwa uweje na upambike kwa sifa zipi?.

Mifano ya Sifa za Kimaadili Zinazofaa Kusifika Nazo:

  1. Sifa ya Uadilifu: Hapa tunajiuliza swali la msingi: Je, Muislamu unatakiwa kusifika kwa sifa ya Uadilifu au unatakiwa kusifika kwa sifa dhulma (kudhulumu haki za watu)?. Hili linahusiana na sifa ya mtu, hivyo ni suala la kimaadili. Uislamu unatufundisha kwamba Muislamu anatakiwa asifike kwa sifa za uadilifu, na asisifike kwa sifa za dhulma ya aina yoyote ile, sawa sawa iwe ni dhulma ndogo au kubwa, au dhulma ya daraja la chini au daraja la juu, wewe kama Muislamu hutakiwi kusifika na dhulma hiyo.
  2. Sifa ya Ushujaa: Ushujaa ni moja ya sifa nzuri kwa Muislamu. Uislamu unatuhimiza na kutufunza sisi kwama Waislamu kuwa tujipambe kwa sifa ya ushujaa. Ushujaa huo unaweza kuwa katika rai, katika misimamo sahihi na ya haki, katika vita, na katika sehemu mbalimbali ambapo panaweza kuhitajia Muislamu uwe shujaa. Kwa hiyo sifa ya Ushujaa ni sifa nzuri ambayo Muislamu anatakiwa apambike nayo.
  3. Sifa ya Ukarimu: Uislamu unamuhimiza Muislamu kujipamba kwa sifa ya Ukarimu. Kwa hakika sifa hii ni sifa nzuri inayompamba Muislamu na Mwanadamu yeyote anayezingatia ukarimu kwa kwatu.

Mifano ya Sifa Mbaya Dhidi ya Maadili Zisizofaa Kusifika Nazo:

  1. Sifa ya Unafiki: Uislamu umekataza sifa ya unafiki. Sifa ya Unafiki sio sifa nzuri bali haipendezi kwa Muislamu. Uislamu umetufunza kwamba miongoni mwa sifa mbaya kupindukia kwa Mwanadamu na hususan kwa Muislamu, ni kusifika kwa sifa ya Unafiki. Mtu yeyote atakayesifika na sifa hii katika Jamii, kwanza kabisa: Maisha yake hayatakuwa mazuri, kwa sababu sifa ya unafiki ni sawa na sifa ya khiana. Watu wote katika jamii wenye akili timamu, wanapomuona mtu ambaye ni mnafiki, humuepuka au huamiliana naye kwa tahadhari kubwa sana. Pili: Kesho siku ya Kiyama mnafiki yeyote atapata adhabu kali ya Mwenyezi Mungu, na Qur’an Tukufu inasema kuwa wanafiki watakuwa katika tabaka la chini kabisa la Moto wa Jahannam.
  2. Sifa ya Woga: Sehemu ambayo unatakiwa uwe ni shujaa, hujitokezi na unarudi nyuma. Hii ni moja ya sifa mbaya ambazo hazipendezi kwa Muislamu au mtu yeyote.

Mwisho: Hojjat al-Islamu wal-Muslimin, Sheikh Abdul Majid Naser, amehitimisha darsa lake kwa natija hii kwamba: Muislamu yeyote, katika maisha yake yote, ikiwa atazingatia na kuwa makini na pande hizi tatu za Hukumu za Kisheria, akawa na itikadi sahihi zilizojengeka katika msingi wa dalili madhubuti, na matendo yake yakaendana na Hukumu za Kisheria na za Kifiq ya Kiislamu (kulingana na Fat’wa za Marjii au Mujtahdi yeyote anayemfuata), kisha sifa zake za kimaadili zikawa ni sifa nzuri kwa mujimu wa Uislamu, huyo atakuwa amefanya la maana na anaweza kujivuna kuwa amefaulu Duniani na Akhera, kwa sababu atakuwa amefuata mfumo ambao Qur’an Tukufu imetuletea, mfumo ambao tumejifunza kutoka kwenye Sunna za Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w) na Maimam wetu watukufu (a.s).

Wassalam Alaikum wa Rahmatullah Warabarakatuh.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha

Comments

  • Jijjan TZ 18:11 - 2025/02/28
    Good