Kulingana na ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Hayati Ayatollah Mohammad Ali Naseri, mmoja wa Maprofesa wa Maadili wa Hawza, alijadili mada isemayo kuwa: "Wilayat, ni Mhimili wa kukubalika kwa matendo" katika moja ya masomo yake ya Maadili (Akhlaq), ambapo maandiko yake ni haya ifuatavyo:
Imamu Sajjad (amani iwe juu yake), anasoma Munajati katika moja ya Dua za Makarim al-Akhlaq / Maadili Mema kama ifuatavyo:
«اللهُمَّ اسْلُكْ بِي الطَّرِیقَةَ المُثْلی»
Maana yake: "Eeh Mola wangu!, niongoze katika njia iliyo bora."
Uislamu unategemea nguzo tano za kimsingi zifuatazo:
1. Swala: Nguzo ya Dini na kigezo cha kukubalika kwa (amali) matendo mengine.
2. Kufunga: Funga ni sababu ya kuimarisha Ucha-Mungu na kujiboresha (kinafsi).
3. Zakat: Ikijumuisha Zaka ya Mali, Zakatul_Fitri, na dhana pana ya ukuaji na ubora.
4. Hajji: Ibada ya Hijja ni ishara ya Umoja na Ibada ya pamoja ya Waislamu.
5. Wilayat: Ni mhimili Mkuu na sharti la kukubalika kwa matendo yote (amali zote).
Miongoni mwa nguzo hizo, Wilayat ya Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao) ina nafasi maalum. Nafasi hii maalum inatokana na uhusiano uliopo wa moja kwa moja wa Maimamu na Ulimwengu wa Wahyi na mambo ya hakika ya Mwenyezi Mungu(s.w.t).
Katika Usiku wa Lailatul_Qadr, Malaika wa Roho humshukia Imam wa Zama (amani iwe juu yake), na uhusiano huu wa kiungu unaendelea. Allamah Majlisi amesimulia riwaya 71 katika kuunga mkono jambo hili katika Juzuu ya 27 ndani ya Bihar al-An'war.
Katika Hadithi yenye mlolongo wa sanadi inayotegemewa, imepokewa kutoka kwa Imamu Sadiq (amani iwe juu yake) kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w) ananukuu maneno ya Malaika Jibril (a.s) yasemayo kuwa:
Mwenyezi Mungu anasema: Nimeziumba Mbingu Saba na Ardhi Saba na viumbe vyote, na sikuumba (eneo) mahali ambapo pana utukufu wa juu zaidi kuliko mahali (eneo) la "rukni na makam"; Lakini ikiwa mja ataabudu (atafanya ibada) katika sehemu hii takatifu zaidi tangu mwanzo wa uumbaji hadi mwisho na asikubali Wilayat ya Ahlul-Bayt (amani iwe juu yake), mtu huyo makazi yake ya milele yatakuwa motoni.
Usimulizi wa Maisarah pia unathibitisha dhana hii. Alimwambia Imam Sadiq (a.s) kwamba anaamka kutoka usingizini kutokana na Sauti ya Swala ya Jirani yake na aliomba Dua kwa ajili ya kuamka kwake.
Imam (amani iwe juu yake) baada ya kuulizwa juu ya imani ya jirani huyo kuelekea Wilayat, alijibu akisema: “Hata kama mtu ataabudu kwa muda wa miaka elfu moja katika sehemu takatifu zaidi duniani (Baina ya Rukni na Maqam, na baina ya Kaburi na Mimbari ya Mtume), lakini bila ya kuikubali Wilayat ya Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao), huyo hatakuwa na mwisho wowote ispokuwa Jahannamu".
Kwa kuzingatia baraka hii kuu ya kimungu, inafaa kusema kwamba:
1. Tusifiche nuru ya Wilayat kwa kutenda dhambi na kufuata matamanio ya nafsi.
2. Tuzingatie Swala ya Usiku, ambayo inapelekea kufunguka kwa riziki na kuimarisha Wilayat.
3. Hata kama hatuwezi kusimamisha kikamilifu Swala ya Usiku, basi tunapaswa kutekeleza angalau rakaa tatu za Witri.
4. Kushikamana na Swala ya Usiku, kunapelekea kukamilika kwa Wilayat, kukuepusha na dhambi na kukukinga na vishawishi vya kimwili na vya kishetani.
Your Comment